MHE.RAIS SAMIA KUONGOZA TROIKA SADC NOV 20 ZIMBABWE

 

MHE.RAIS SAMIA KUONGOZA TROIKA SADC NOV 20 ZIMBABWE

MHE.RAIS SAMIA KUONGOZA TROIKA SADC NOV 20 ZIMBABWE

TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC  Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa Kilele wa Troika wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika Jumatano Novemba 20, 2024 mjini Harare, Zimbabwe.
Mkutano wa Troika utatanguliwa  na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC, ambao unakusudia kuhakiki hali ya usalama katika kanda hiyo, kwa kuzingatia hali ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Sekretarieti ya SADC, Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utaongozwa na Rais wa Zimbabwe Dk Emmerson Mnangagwa, mwenyekiti wa kanda ya Kusini.
Mkutano huo utapokea taarifa kuhusu maendeleo ya Ujumbe wa SADC katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC),” ilisomeka taarifa hiyo.
SAMIDRC ilitumwa Desemba 15, 2023 kwa muda wa mwaka mmoja kama jibu la kikanda la kukabiliana na hali ya usalama nchini DRC na kurejesha amani, usalama na utulivu ili kuandaa njia ya maendeleo endelevu.
Pia, Mkutano wa Troika utatanguliwa na vikao vya Viongozi Waandamizi wa SADC, Kamati ya Mawaziri ya Chombo cha Siasa Ulinzi na Ushirikiano wa Usalama na Baraza na Baraza la Mawaziri la SADC.
SADC ni jumuiya ya nchi wanachama 16 iliyoanzishwa mwaka 1980 kama Mkutano wa Uratibu wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADCC) na baadaye Agosti 1992 ilibadilishwa kuwa SADC.