TSH BIL 1 ZAFIKISHA MAJI CHITOHOLI,MKUNDI,CHIKONGOLA
MTWARA
Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujengaji wa tanki lenye ujazo wa lita 225,000 juu ya ardhi katika mradi wa maji wa Chitoholi ambao utahudumia wakazi wapatao 10,817 wa vijiji sita vilivyopo kwenye kata ya Mkundi na Chikongola katika halmashauri ya wilaya Tandahimba Mkoani Mtwara.
Mradi huo umetekelezwa ili kutatua adha ya upatikanaji wa maji safi na salama ambapo hapo awali walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 5 hadi 8 kufuata maji.
Pia katika mradi huo umefanyika ujenzi wa vioski 15, ujenzi nyumba ya pampu pamoja na kuunganisha huduma ya maji katika taasisi saba ambazo ni zahanati na shule pamoja na mengine.
Miongoni mwa wakazi wa vijiji hivyo ambao ni wanufaika wa mradi huo akiwemo bwana Fadhiri Kaumbata mkazi wa kijiji cha Chitoholi ‘A’ wilayani humo amesema wameupokea mradi kwa mikono miwili na kuahidi kulinda miundombinu ya mradi huo.
“Tumeupokea vizuri mradi huu kwani hapo mwanzo ilitulazimu kuamka saa 9 au saa 10 kwa ajili ya kufuata maji hivyo tutahakikisha tunautunza na kuulinda ili tuzidi kunufaika nao”amesema.
