BIL 68.5 KUJENGA BARABARA DODOMA
DAR ES SALAAM
Serikali ya Tanzania na Japan zimesaini mkataba wa makubaliano ya ruzuku yenye thamani ya Yen bilioni 4.07 (takriban shilingi bilioni 68.5/-) kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Ndani ya Jiji la Dodoma, hatua ambayo inalenga kuimarisha mtiririko wa magari na kuboresha mazingira ya kuishi katika mji mkuu. Hafla ya kusaini mkataba imefanyika jijini Dar es salaam Alhamisi,oktoba 17, 2024.
Mradi huu unahusisha kujenga takriban kilomita 3.1 za barabara mpya na kupanua kilomita 3.4 kati ya zilizopo.
Mpango huu umeundwa ili kurahisisha ugavi, kuboresha mtiririko wa trafiki na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika jiji la Dodoma.
Vipengele muhimu vya makubaliano ni pamoja na kujenga njia nne kutoka Mzunguko wa Makulu, pamoja na kupanua mkondo wa njia mbili uliopo kutoka Mzunguko wa Bahi hadi Mzunguko wa Picha kuwa njia nne.
Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuleta mazingira ya kisasa zaidi, yenye ufanisi na endelevu katika jiji la Dodoma pia utaimarisha miundombinu ya jiji na kusaidia ukuaji wa Ukanda wa Kati.
ZINGATIA:- Miradi iliyofadhiliwa inaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22 – 2025/26), ambao unalenga katika kuongeza ushindani na maendeleo ya viwanda kwa maendeleo ya watu kwa kuongeza ufanisi na tija kwa rasilimali zilizopo.
