TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA EU, UNDP, SADC
ARUSHA
Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) , Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland imeandaa Mkutano wa Kikanda kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unaohusu masuala ya Matumizi Bora ya Nishati.
Mkutano huo utakaofanyika tarehe 4-5 Desemba 2024, jijini Arusha unatokana na programu ya pamoja ya Serikali ya Tanzania, UNDP, EU na Ubalozi wa Ireland inayohusika na Matumizi Bora ya Nishati iliyoanza kutekelezwa mwaka 2022.
Mkutano huo, ujulikanao kama Regional Energy Efficiency Conference (REEC) unahusisha wadau wa nishati takriban 400 wa ngazi mbalimbali ikiwemo Mawaziri, wataalam na sekta binafsi, utajumuisha kubadilishana uzoefu na uelewa katika masuala ya nishati, fursa zilizopo na uwekezaji.
Naibu Balozi wa Ireland nchini, Mags Gaynor amesema Ubalozi huo unafurahishwa na jinsi Tanzania inavyotekeleza Programu ya Matumizi Bora ya Nishati ikiwemo kuandaa mkakati utakaopelekea Tanzania kutekeleza kwa ufanisi zaidi programu husika.
Akizungumzia Mkutano huo wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati, amesema ni hatua kubwa katika safari ya mabadiliko kuelekea kwenye matumizi bora ya nishati pamoja na kuwa njia ya kusukuma ajenda ya matumizi bora ya nishati.
Kwa upande wake, Programu Meneja wa Miradi ya Nishati kutoka EU, Massimiliano Pedretti ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa programu hiyo ambayo imeonesha mafanikio makubwa na kueleza kuwa Umoja huo utaongeza muda wa utekelezaji wa programu hiyo nchini ambayo ilikuwa ikifikia ukomo mwaka huu wa 2024 lakini sasa itaisha mwaka 2025 pamoja na kutanua wigo wa kazi pamoja na ufadhili.
Naye, Abbas Kitogo, Mtaalam wa Miradi kutoka UNDP, amesema Mkutano huo wa kikanda, utakuwa ni sehemu ya kubadilishana ujuzi, uelewa na kuhakikisha kunakuwa na uelekeo mmoja katika matumizi bora ya nishati kwani kila mmoja akifanya juhudi matumizi ya nishati isiyo salama yanatupungua na kuelekezwa kwenye sehemu zenye uhitaji na kupunguza gharama za nishati ambazo zinaweza kuelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.